Image

Tatizo la kunyonyoka nywele hujulikana kitaalamu kama alopecia (tamka ‘’ alopesia’’). Hali hii ya kunyonyoka nywele husabababishwa na mfumo wa kinga ya mwili kushambulia mwili wa mtu husika (autoimmune disorder).

Kwenye alopecia, mfumo wa kinga ya mwili hushambulia mizizi ya nywele (hair follicles) na hivyo kusababisha kunyonyoka kwa nywele.

Wingi wa kunyonyoka nywele hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.Kwa baadhi ya watu, nywele hunyonyoka sehemu ndogo na kusababisha mabaka mabaka madogo ambayo mwanzoni sio rahisi mtu kugundua.Baadae mabaka haya huungana na kuwa sehemu moja kubwa iliyonyonyoka nywele na hatimaye mtu anaweza kugundua.

Kwa wengine, nywele hunyonyoka kwa wingi sana. Baadhi ya wagonjwa wameota  nywele baada ya awali kunyonyoka na kisha nywele hizo hunyonyoka tena. Mara chache hutokea kwa mgonjwa alienyonyoka nywele kuota tena nywele hizo kwa maisha yake yote.

Alopecia haina uhusiano wa umri wala jinsia ya mtu.Kwa hiyo, mtu yoyote anaweza kupata hali hii.

Naweza Kunywa Pombe kama nina Ugonjwa wa kisukari?

Wagonjwa wengi wa kisukari wameniuliza kuhusu swali hili.Aghalabu, hata wengine ambao wanasoma makala hii pia watakuwa na shauku ya kutaka kujua kama kweli wanaweza kunywa pombe ilihali wanaugua ugonjwa wa kisukari bila kupata madhara yoyote ya afya.Swali hili ni la msingi sana hasa unapokuwa kwenye matibabu ya ugonjwa wa kisukari.

Ugonjwa wa kisukari ni moja kati ya magonjwa mengi yasiyoambukiza (non-communicable diseases) ambayo yanongezeka kwa kasi na kusababisha vifo na ulemavu.

Taarifa ya International Diabetes Federation imesema watu millioni 463 duniani wanaishi na kisukari na millioni 19 ya hao wapo bara la Afrika pekee.

Shirika hili katika taarifa yake ya mwaka 2020 limesema kwamba uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari  nchini Tanzania ni kwa asilimia 3.7 huku idadi ya wagonjwa wa kisukari watu wazima imefika takribani watu 997,400.

Unywaji wa pombe uliopitiliza kwa watu wenye kisukari husababisha madhara makubwa ikiwemo kuongeza hatari ya kupata shinikizo la damu, magonjwa ya moyo,macho na kuharibika kwa mishipa ya fahamu.

Aidha Pombe au vileo vingi vina idadi kubwa ya wanga na sukari hivyo husababisha kupanda kwa haraka kwa sukari kwenye damu. Pia vina kalori nyingi hii upelekea kuwepo hatari ya kuongezeka uzito uliopitiliza ambapo hupunguza unyeti (sensitivity) na utolewaji wa kichocheo aina ya insulin  mwishowe husababisha ugumu wa kudhibiti sukari yako mwilini.

Sasa je naweza kunywa pombe kama ni ugonjwa wa kisukari?

jibu ni NDIO japo inabidi ujenge tabia ya kuwa na tahadhari pindi unapokunywa pombe.

Utatumia pombe pale tu ambapo sukari yako imedhibitiwa vizuri na kwa hali yoyote epuka unywaji pombe kupitiliza.

Najua kuna swali unaliwaza kuwa nisinywe kupitiliza unaamanisha nini?

Hili ni swali zuri na la msingi.Kulingana na shirika la ugonjwa wa kisukari la marekani (American Dabetes Association), imetoa vipimo vifuatavyo vya unywaji wa pombe kwa watu wenye kisukari.

Mwanamke mwenye kisukari asinywe zaidi ya chupa moja ya bia  sawa na 350mls, au 147 mls za wine na 44 mls za pombe kali kwa siku.

Kwa mwanamume, asinywe zaidi ya bia mbili sawa na 700mls, au 294 mls za wine au  88 mls za pombe kali.

USHAURI

Kabla ya kunywa pombe hebu jiulize masawali yafuatayo;

Je sukari yangu imedhibitiwa?

Je daktari wangu anakubali nitumie pombe au kilevi cha aina yoyote ile?

Je najua jinsi pombe inaweza kuniathiri mimi pamoja na sukari yangu?

Kama majibu yako yote ni ndio basi waweza kunywa pombe. Ila kumbuka pombe pia husababisha sukari kushuka. Ni vizuri kufahamu kiwango cha sukari yako mwilini kabla, wakati na baada ya kunywa pombe angalau kwa kipindi cha masaa 12.

Usikose kutembelea TanZMED kwa makala zaidi za afya kwa lugha ya kiswahili.

 

Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu zinazojulikana kitaalamu kama bronchioles.

Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko mwili sugu (chronic Inflammation) kwenye mirija yake ya kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii, kujaa kwa ute mzito (mucus) na kupungua kwa njia ya kupitishia hewa, hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa nje na hivyo kupumua kwa shida sana. Hali hii inaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu.

Kutokana na  kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua  nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease . Mtu aliye na pumu, huwa nayo kipindi chote cha maisha yake.  

Makundi ya Pumu

Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili;

  • Pumu ya ghafla (Acute asthma):  Wagonjwa wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida  katika njia zao za hewa isiyobadilika kati ya shambulizi moja na jingine.
  • Pumu sugu (Chronic Asthma): Kundi hili la pumu huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa  na kadiri jinsi mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu, njia za hewa huzidi kuwa nyembamba zaidi.

Aina za ugonjwa wa pumu

Bila kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni

1.Pumu inayobadilika (brittle asthma): Kulingana na tabia ya kujirudia rudia kwa matukio ta ugonjwa huu na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili, ambazo ni

  • Aina ya kwanza ya pumu inayobadilika (type 1 brittle asthma) ni pumu yenye tabia ya kuwa na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.
  • Aina ya pili ya pumu inayobadilika (type 2 brittle asthma)  ni pumu ambayo mgonjwa anatokea kupata shambulizi la ghafla (asthmatic attack) wakati hapo awali ugonjwa wake uliweza kuthibitiwa kwa matibabu.

 

Maana ya Kiharusi

Kiharusi ni hali inayotokea pale mishipa inayosambaza damu kwenye ubongo inapopatwa na misukosuko kiasi cha kushindwa kupeleka damu kwenye ubongo na hivyo kuathiri ufanyaji kazi wa ubongo kwa zaidi ya masaa 24.

Kulingana na shirika la afya duniani kiharusi ni nakisi katika neva ambayo hutokana na tatizo katika mishipa ya damu ya ubongo na ambalo huendelea zaidi ya masaa 24 au kukoma ndani ya masaa 24. Muda wa masaa 24 umechukuliwa ili kutofautisha kiharusi na kiharusi cha kukosa oksijeni katika ubongo (ischemia) ambacho hutokea na kudumu kwa muda mfupi yaani (transient ischemic attack).

Kwa kawaida dalili za TIA hupotea na mtu kurudia hali yake ya kawaida ndani ya masaa 24.

Aina za kiharusi

Kiharusi kimegawanyika katika aina kuu mbili kulingana na jinsi kinavyotokea (visababishi vyake). Aina hizo ni

Kiharusi cha kukosa hewa kwenye Ubongo (Ischemic stroke)

Aina hii ya kiharusi hutokea iwapo usambazaji wa damu katika sehemu ya  ubongo hupungua na kupelekea tishu za ubongo za eneo liliathirika kushindwa kufanya kazi zake vizuri.

Aina hii ya kiharusi husababishwa na nini?

  • Damu iliyoganda kuziba mishipa midogo ndani ya ubongo (cerebral thrombosis) au
  • Kipande cha damu kumeguka na kwenda kuziba mshipa wa damu kwenye ubongo(cerebral embolism)
  • Kupungua kwa usambazaji wa damu kwa ujumla kwa mfano shock.
  • Vena thrombosis

Kiharusi cha kuvuja damu ndani ya Ubongo (Haemorrhagic Stroke)

Aina hii ya kiharusi hutokea pale ambapo mishipa midogo ya damu ndani ya ubongo hupasuka na kusababisha kusambaa kwa damu ubongoni (cerebral hemorrhage). Mara nyingi aina hii ya kiharusi hutanguliwa na dalili za kichwa kuuma, au kuwepo kwa historia ya ajali ya kichwa.

Visababishi vya Kiharusi (kwa ujumla)

  • Wakati fulani, mishipa ya damu huzungukwa na aina fulani za mafuta yasiyofaa mwili, hali inayoitwa kitaalamu kama atherosclerotic plaque. Hali hii husababisha kuganda kwa damu katika mishipa (thrombosis) hiyo. Kuganda huku kwa damu kunaweza kutokea kwenye mishipa mikubwa au midogo inayopeleka damu kwenye ubongo. Baadhi ya mishipa mikubwa ya damu inayoweza kuathirika na tatizo hili ni pamoja na arteri za common carotid na interior carotid arteries, na arteri za vertebral. Nyingine ni mishipa midogo inayounda eneo linaloitwa circle of willis lililo katika ubongo.
  • Kuganda kwa chembe nyekundu za damu za mgojwa wa sickle cell kunaweza pia kusababisha kuziba mishipa ya damu hivyo kusababisha Kiharusi.
  • Kuganda kwa damu (embolus) kwenye mishipa ya damu ya sehemu nyingine za mwili au (hewa, mafuta, kusanyiko la vijimelea kama bakteria waletao ugonjwa wa endocarditis) huweza kusababisha kuziba kwa mishipa inayosambaza damu kwenye ubongo na hivyo kusababisha kiharusi.
  • Upungufu wa usafirishaji damu mwilini (systemic hypoperfusion) - Wakati fulani moyo hushindwa kusukuma damu vizuri kwenda sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo ubongo kutokana na kufa kwa sehemu za nyama ya moyo kwa kukosa damu ya kutosha (Ischaemic Heart Diseases) au kutokana na kujaa kwa maji kwenye gamba lake la nje (pericardial effusion) au kupungua kwa damu mwilini, kunakoweza kusababishwa na mambo kadhaa. Hali hii husababisha sehemu kubwa ya mwili ikiwemo ubongo kukosa oksijeni ya kutosha na kusababisha kuathiriwa kwa sehemu ya ubongo.
  • Shinikizo la damu la muda mrefu lisilothibitiwa linaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa midogo inayosambaza damu kwenye ubongo na hivyo damu kujaa kwenye ubongo (Intracerebral hemorrhage).

Dalili za kiharusi

Dalili za kiharusi hutegemea na eneo la ubongo liliathiriwa.

  • Iwapo sehemu ya ubongo mkubwa ( Cerebellum) itaadhirika, mgonjwa atakuwa na dalili kama kushindwa kutembea vizuri, hivyo kuathiri mwendo wake, kujihisi kizunguzungu na pia kutapika.
  • Iwapo sehemu ya ubongo wa kati (cerebral cortex) itakuwa imeathirika, mgonjwa atakuwa na dalili za kushindwa kuongea,kushindwa kuelewa lugha inayozungumzwa, kushindwa kuona vizuri, kuwa na ukosefu wa kumbukumbu, kuwa na mvurugiko wa mpangilio wakw wa kufikiri, kuchanganyikiwa, na kubadilika kwa mwendo wa harakati za hiari.
  • Iwapo mgonjwa ataadhirika sehemu ya ubongo kwenye shingo kuelekea kwenye uti wa mgongo (brain stem), mgonjwa anaweza kuwa na dalili za kuhisi mabadiliko ya harufu, ladha, kusikia na kuona; kulegea kwa misuli ya macho (ptosis); kupungua kwa ufahamu na kulegea kwa misuli ya uso; Ulegevu wa Ulimi (kushindwa kutoa nje au kusogeza upande upande); kupungua uwezo wa kumeza; ulegevu wa misuli ya shingo na kushindwa kugeuza shingo upande mmoja; kushindwa kusimama sawasawa na kuona vitu kwa hali ya utofauti; mabadiliko ya upumuaji na kiwango cha moyo kudunda.
  • Iwapo sehemu mojawapo ya mfumo mkuu wa neva (central nervous system) imeathirika, mgonjwa atakuwa na dalili za kupoteza ufahamu kwa upande mmoja wa mwili na kulegea kwa misuli ya uso, kuhisi ganzi mwilini, na kupungua kwa ufahamu wa hisia na hisia mtetemo.

Aidha bila kujalisha eneo lililoathiriwa, mgonjwa pia anaweza kuwa na dalili za kupoteza fahamu, maumivu makali ya kichwa na kutapika. Dalili hizi za kuumwa kichwa na kutapika kwa kawaida hutokea kwa mgonjwa mwenye kiharusi cha kuvuja damu (hemorrhagic stroke) ambacho husababisha ongezeko la shinikizo na mgandamizo wa ubongo ndani ya fuvu kutokana na kuvuja kwa damu.

Vipimo

  • Mionzi                                                           
  • CT-scan
  • MRI
  • PET
  • SPECT

Vipimo vingine ni

  • ECG, ECHOCARDIOGRAM huwezesha kutambua hitilafu katika mapigo ya moyo (arrhythmia) na kama kuna damu iliyoganda kwenye moyo ambayo inaweza kufika kwenye ubongo
  • Holter monitor husaidia kutambua hitilafu katika mapigo ya moyo (arrhythmia) zinazotokea kwa vipindi
  • Angiogram huwezesha kugundua matatizo kwenye mishipa ya damu, na ni mishipa ipi ya damu iliyoziba.
  • Vipimo vya damu huwezesha kutambua uwepo wa lijamu mwilini (hypercholesterolemia) na mabadiliko mengine katika damu

Vihatarishi vya kiharusi

Vitu vinavyoweza kumuweka mtu katika hatari ya kupata kiharusi ni pamoja na

  • Shinikizo la damu lisilothibitiwa
  • Kisukari
  • Uvutaji sigara
  • Unywaji pombe kupita kiasi
  • Kutofanya mazoezi kabisa
  • Fetma (obesity)
  • Kuwa na cholesterol nyingi kwenye damu
  • Atrial fibrillation

Matibabu

Matibabu ya kiharusi hutegemea pia aina na visababishi vyake .

Matibabu ya kiharusi kinachotokana na ubongo kukosa hewa (Ischemic stroke)

Mgonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa za kuyeyusha damu iliyoganda (thrombolytics) au kwa kuondoa damu iliyoganda kwa njia mbalimbali (thrombectomy). Dawa nyingine kama vile junior Aspirin na Clopidogrel hutolewa kwa ajili ya kuzuia chembe sahani kukusanyika na kuganda.

Matibabu ya kiharusi kinachotokana na damu kuvujia kwenye ubongo (Hemorrhagic stroke)

Aina hii ya kiharusi huitaji tathmini ya upasuaji wa neva ili kuchunguza na kutibu sababu ya damu kuvuja. Angalizo: ni hatari kumpa mgonjwa wa aina hii ya kiharusi dawa za kuyeyusha damu iliyoganda au za kuzuia kuganda maana uhatarisha maisha ya mgonjwa badal ya kumsaidia. Kwahiyo ni vizuri kwa wataalamu kufanya ufanya uchunguzi wa kutosha ili kuwa na uhakika na tatizo.

Huduma na Matunzo kwa mgonjwa wa Kiharusi

Mojawapo ya mambo muhimu ya kufanya kwa mgonjwa aliyepata kiharusi ni kumuongoza na kumuelimisha ili arudishe ujuzi wake wa maisha ya kila siku. Hapa uhitaji ushirikiano wa wauguzi, wataalamu wa viungo, wataalamu wa ushauri wa kazi na daktari. Kuna umuhimu pia wa kuwaelimisha ndugu kuhusu hali ya mgonjwa ili waweze kumsaidia katika matunzo yake nyumbani na kwenye jamii inayomzunguka.

Matarajio (prognosis)

Asilimia 75 ya wagonjwa wa kiharusi wanaonusurika kifo huwa walemavu na kusababisha kuathirika kwa ufanyaji kazi wao na kuajiriwa. Ulemavu unaweza kuwa wa kimwili au kiakili au vyote kwa pamoja.

Ulemavu wa kimwili ni pamoja na

  • Ulegevu wa misuli
  • Kujihisi ganzi sehemu mbalimbali za mwili hususani zilizoathirika
  • Kujikojolea
  • Kutoona vizuri
  • Kushindwa kuendelea na shughuli za kila siku
  • Vichomi
  • Vidonda shinikizo
  • Kukosa hamu ya chakula.

Ulemavu wa akili hujumuisha vitu kama

  • Mgonjwa kuwa na wasiwasi
  • Hofu ya mashambulizi, na
  • Unyongovu.

Jinsi ya kuzuia kiharusi

  • Zuia au tibu shinikizo la damu
  • Dhibiti kisukari
  • Fanya mazoezi
  • Acha kuvuta sigara
  • Punguza uzito
  • Acha kunywa pombe kupita kiasi
  • Tumia Junior Aspirin
  • Kula chakula kisichokuwa na mafuta mengi na kisicho na chumvi nyingi.
  • Tumia dawa za kupunguza mafuta mwilini (statins)kwa mfano Simvastatin

Ni tatizo ambalo huathiri wote wanaume na wanawake, vilevile watu wa rika yote kwa ujumla. Tatizo hili husababishwa na mpasuko au mchaniko katika eneo la mwisho la mfereji wa haja kubwa.

Nini husababisha mwatuko wa mfereji wa haja kubwa?

Aina yoyote ya ajali katika mfereji wa haja kubwa husababisha mwatuko kama ifuatavyo:

  • Kupata choo kingi na kigumu kwa muda mrefu
  • Tatizo sugu la kuharisha
  • Kuvimba kwa eneo la mfereji wa haja kubwa (inflammation)

Sababu nyinginezo ni kama zifuatazo

  • Ngono ya njia ya haja kubwa
  • Kansa
  • Virusi vya ukimwi
  • Kaswende
  • Kifua kikuu

Watu gani wanaweza kupata tatizo hili?

  • Watoto chini ya mwaka mmoja (infants)
  • Umri mkubwa- kwasababu kuna upungufu wa ugavi wa damu katika mfereji wa njia ya haja kubwa
  • Kupata choo kigumu kwa muda
  • Wanawake wakati wa kujifungua
  • Crohn’s disease

Dalili

  • Maumivu mara baada ya haja kubwa
  • Damu kwenye kinyesi na huonekana kwenye karatasi ya chooni (toilet paper)
  • Maumivu huweza kuwa makali mpaka kumfanya mtu ajizuie kwenda msalani
  • Kuwashwa

Vipimo na uchunguzi

  • Sigmoidocopy
  • Colonoscopy

Matibabu

Huweza kutibiwa kwa dawa katika hatua za awali

  • Dawa za kulainisha choo
  • Sitz bath
  • Cream za kupaka (Anusol, zinc oxide)
  • Nitroglycerin
  • Botox
  • Calcium channel blockers (nifedipine and diltiazem)

Kama tatizo hili limekuwa sugu na halitibiki kwa tiba nyingine, basi Upasuaji ndio huwa tiba mwafaka

  • Partial lateral internal sphicterotomy
  • Anal dilation

Jinsi ya kuzuia mwatuko wa mfereji wa haja kubwa

  • Vyakula vya kulainisha choo - matunda na mbogamboga
  • Kunywa maji mara kwa mara
  • Na fanya mazoezi

Ni ugonjwa unaoshambulia ini na husababishwa na virusi au bacteria wa aina za A, B, C, D

Na vile vile huweza kusababishwa na :

  • Fangasi
  • Unywaji wa pombe (alcoholic hepatitis)
  • Dawa
  • Magonjwa yanayosababishwa na kinga ya mwili kuushambulia mwili (autoimmune)
  • Magonjwa ya kimetaboliki

Magonjwa yanayosababiswa na virusi au bacteria husambazwa kutokana na aina zake:

Homa ya Ini isababishwao na aina A (Hepatitis A), E

  • Kwa kula kinyesi kilichochanganyika na aina hii ya vimelea kwenye Maji, chakula

Homa ya Ini isababishwao na aina B (hepatitis B), C, D, G

  • Mchanganyiko wa damu ambao hutokana na:
    • Ngono zembe
    • Kutumia Sindano zilikwishatumika wakati wa matumizi ya madawa ya kulevya
    • Wakati wa kuwekewa damu
    • Kwenye kusafisha figo kwa wenye shida za figo

Mwaka 2013 virusi vya homa ya ini vilishika nafasi ya saba kwenye sababu ya vifo duniani,  mara nyingi homa ya Ini husababishwa na virusi zaidi ya hizo sababu nyingine.

Na homa ya ini imeganwanyika kama ifuatavyo

  • Ya hapo kwa papo kitaalamu acute hepatitis
  • Sugu kitaalamu chronic hepatitis

Dalili za Homa ya Ini

Kwa wagonjwa wengine wanaweza kukaa bila dalili mpaka madhara ya ugonjwa huu yanapoathiri ini.

Dalili ambazo hutokea ni:

  • Kichefuchefu
  • Kutapika
  • Ladha kubadilika mdomoni
  • Kupoteza hamu ya kula
  • Uchovu
  • Kuwashwa
  • Kukojoa mkojo mweusi
  • Maumivu ya tumbo upande wa juu wa kulia
  • Manjano kuonekana kwenye viganja vya mkono na machoni
  • Maumivu ya misuli na viungo
  • Homa

Madhara ambayo yanaweza kutokea baada ya kuugua homa ya Ini

  • Ini kuoza (hepatic necrosis)
  • Ini kukakamaa na kuota vinundunundu (cirrhosis)
  • Ini kushindwa kufanya kazi (hepatic failure)
  • Saratani ya Ini (hepatocellular carcinoma)

Vipimo

  1. Maabara
  • Kipimo cha damu kujua aina ya homa ya ini
  • Kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa ini, kupitia kuangalia vimenge’nyo vya kwenye ini
  1. Picha
  • Kipimo cha kuangalia ini kitaalamu ultrasound

Tiba

Ni vyema kwenda hospitali na kufanyiwa uchunguzi kusudi upewe dawa na matibabu muhimu.

Baadhi ya wagonjwa huweza kunufaika na matibabu ya dawa, na madhumuni ya dawa ni kuzuia kuendelea kuathirika kwa ini

Dawa ambazo mgonjwa hupewa kitaalamu ni: ( interferons [IFNs], antivirals, and corticosteroids)

Lamivudine na Adenofir zimeonyesha matokeo ya kuaminika kwenye matibabu ya homa ya ini aina B.

 

 

Usonji ni tatizo linalojitokeza mapema utotoni, ambapo mtoto huwa na mapungufu kwa kupenda kujitenga na kutotaka kuwa karibu na watu (Impaired social interaction), hupata matatizo ya lugha na shida ya mawasiliano (impaired language and communication skills) na huwa na  tabia ya kurudia rudia kitu anachokifanya mara nyingi (restrictive repetitive behaviour).

Mara nyingi wazazi hugundua watoto wao wana tatizo hili katika kipindi cha  miaka miwili ya umri wa mtoto.Chanzo halisi cha tatizo hili la usonji hakijulikani ingawa  matatizo ya kijenetiki (Neurodevelopmental disorder) ndio uhusishwa na tatizo la usonji.Maaambukizi ya Rubella  au matumizi ya pombe na madawa ya kulevya aina ya coccaine wakati wa ujauzito na hata sababu za kimazingira, yote haya  uhusishwa na tatizo hili la usonji.

Watoto wa kiume huathirika sana ikilinganishwa na watoto wa kike. Kwa kila watoto watatu wa kiume wenye kupata usonji ni mtoto mmoja tu wa kike anaepata usonji.

Jarida la The Lancent la mwaka 2013, linasema watu wapatao milioni 21.7 wameathirika  kwa tatizo hili la usonji  ulimwenguni kote 1. Tabia za kujirudia rudia kwa mtoto aliyeathirika na tatizo la usonji zimegawanyika katika makundi yafuatayo;

  • Tabia zilizozoeleka - Kama  kupiga piga mikono, kutikisa tikisa kichwa mara kwa mara na kujibiringisha mwili
  • Tabia ambazo huchukua sana muda kama za kupanga panga vitu kwa mpangilio maalum au kuosha mikono mara kwa mara
  • Tabia ya kung’ang’ania vitu visihamishwe kwa mfano viti au kutokubali kukatizwa katizwa

Ugunduzi (Diagnosis)

Ugunduzi wa tatizo hili la usonji hufanyika kwa

  • Daktari wa watoto  (Pediatrician) kumpima vipimo vya kawaida pamoja  na kuchukua historia ya  ukuaji wa mtoto husika (Developmental milestones)
  • Daktari bingwa wa watoto aliyebobea kwenye matatizo ya kisaikolojia ya watoto (Pediatric neuropsychologists) kumpima ili kuangalia tabia za mtoto huyu  na uwezo wake wa kiakili (Cognitive skills)
  • Vipimo vya kijenitikia (genetics testing) kama high-resolution chromosome and  fragile X testing. Hufanyika baada ya   kugundulika kwamba chanzo cha  tatizo la usonji ni matatizo ya kijenetiki

Kadri mtoto anavyoendelea kukuwa ndio usonji unavyoweza kutambulika kwa urahisi zaidi kwani madhara yake yanaonekana kwa urahisi wakati wa  ukuaji wa kiakili wa mtoto.

Uchunguzi

Mchunguze mtoto wako kwa viashiria vya tatizo la usonji mapema zaidi kwani kumchelewesha mtoto mwenye usonji kupimwa na kupewa tiba mapema huchangia tatizo hili kuwa kubwa zaidi na hivyo kuathiri matokeo ya matibabu ya tatizo hili. Nusu ya wazazi hugundua watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya miezi 18 ya umri wa mtoto, na moja ya tano ya wazazi hugundua ya kwamba watoto wao wana tabia zisizo za kawaida ndani ya kipindi cha miezi 24 ya umri wa mtoto 2.Tabia hizi ambazo si za kawaida katika ukuaji wa mtoto ni;

  • Kutotamka maneno ya kitoto (no babbling)  mpaka anapotimiza umri wa mwaka mmoja
  • Kushindwa kuotesha kidole au kumpungia (waving, gesturing etc) mzazi/mtu yoyote mkono mpaka anapotimiza umri wa miezi 12
  • Kushindwa kutamka neno lolote mpaka anapotimiza umri wa miezi 16
  • Kutotamka maneno mawili kwa pamoja au sentensi mpaka umri wa miezi 24
  • Kupoteza uwezo wa kuongea au kutokuwa na tabia ya kutangamana/kuchanganyikana na watu wengine wakati wowote ule katika umri wa mtoto

Matibabu

Familia yenye mtoto mwenye tatizo la usonji huhitaji kuelemishwa jinsi ya kuishi na mtoto huyo pamoja na kusaidiwa katika malezi yake. Kwa kuwa tatizo hili  halitibiki ni muhimu mtoto kupata:

  • Tiba ya Tabia
    • Uchambuzi wa tabia (ABA): Kutumia utaalamu wa kisaikolojia kufundishia na kuwahusisha na jamii, kuboresha mawasiliano, na usimamizi wa kitabia
    • Matibabu na elimu ya usonji kwa kuboresha mawasiliano kwa watoto wenye ulemavu (TEACCH)
  • Tiba nyingine muhimu ni kuelimisha jamii kuhusu watoto wenye usonji , jinsi ya kuishi nao na kuwaanzishia watoto wenye usonji matibabu mapema. 

 

Marejeo

  1. Global Burden of Disease Study 2013 Collaborators (2015)."Global, regional, and national incidence, prevalence, and years lived with disability for 301 acute and chronic diseases and injuries in 188 countries, 1990–2013: a systematic analysis for the Global Burden of Disease Study 2013."Lancet386: 743–800. doi:1016/S0140-6736(15)60692-4PMC 4561509PMID 26063472.
  2. Landa RJ (2008). "Diagnosis of autism spectrum disorders in the first 3 years of life". Nat Clin Pract Neurol. 4 (3): 138–47. doi:10.1038/ncpneuro0731PMID 18253102