Image

"Macho mekundu" ni neno linalotumika kuelezea macho yaliyopata wekundu, kuwasha, na kuwa na viashiria vya damu (bloodshot). Wekundu huu hutokea pindi vimishipa midogo ya damu chini ya uso wa jicho vinapotanuka au kuvimba. Mara nyingi, ni athari ya ukereketaji (irritation) au mashambulizi (infection) ya kwenye jicho. 

Macho mekundu yanaweza kuathiri jicho moja au yote mawili. Pia ni hali ambayo inaweza kutokea taratibu au kwa ghafla, kama vile kwa matatizo ya mzio au jeraha la jicho.

Unaweza kuwa na macho mekundu na dalili nyingine kama vile:

  • Maumivu ya jicho.
  • Kuwasha.
  • Kutokwa na matongotongo.
  • Kuvimba kwa jicho.
  • Mabadiliko katika kuona, kama vile kuona ukungu.

Hatua na viwango tofauti vya ukali wa macho mekundu

Mara nyingi, macho mekundu athari zake huwa kubwa kwa muonekano kuliko jinsi unavyojisikia ndiyo maana kwa wengi huwa hawahisi kitu mpaka wanapoenda kujiangalia na kugundua kuwa jicho limekuwa jekundu. Katika visa vingi, macho mekundu ni ya kawaida na mara nyingi hutibiwa na matibabu ya nyumbani au matibabu ya madawa ya kawaida (OTC).

Lakini ikiwa jicho lako au macho yako yanaendelea kuwa mekundu kwa zaidi ya wiki moja, au una maumivu au matatizo kwenye kuona, hakikisha unaweka miadi ya kuonana na daktari haraka uwezavyo, unaweza kuonana na daktari wa macho ophthalmologist (eye doctor) au daktari wa miwani optometrist.

Ni nini chanzo cha kawaida cha macho mekundu?

Kuna sababu nyingi zinazoweza kupelekea kupata tatizo la macho mekundu, macho yanaweza kupata wekundu kutokana na uvaaji wa lenzi za kuweka machoni kwa muda mrefu au umekaa kwenye kompyuta kwa muda mrefu bila kupata mapumziko. Baadhi ya sababu nyingine za kawaida ni pamoja na:

  • Mzio (Allergies).
  • Tatizo la Blepharitis.
  • Mamabukizi ngozi ya juu ya gololi (Viral Keratoconjunctivitis).
  • Jicho kavu.
  • Jeraha la jicho.
  • Ugonjwa wa Glakoma (Glaucoma).

Mambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu "Viral Keratoconjunctivitis"

Haya ni moja ya maambukizi ambayo hulipuka sana kwenye jamii zetu, Mambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu "Viral Keratoconjunctivitis", ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa. Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba, dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili. Usafi ni jambo muhimu kuzuia maambukizi haya kusambaa kwa watu wengine.  Mlipuko huu husababishwa na Kirusi kijulikanacho kwa jina la Adenovirus kwa asilimia zaidi ya 80%.

Dalili huonekana kuanzia siku 5 hadi 14 baada ya kupata vimelea vya maambukizi. Aidha, mara chache inaweza kuchukua muda mrefu zaidi. Pia, mtu huchukua siku 1 hadi 2 mpaka kuanza kuonesha dalili na anaweza kuendelea kuambukiza takriban wiki mbili baada ya dalili kuanza kuonekana.

Hadi sasa hakuna tiba maalumu kwa maambukizi ya ugonjwa huu, na dalili huisha kwa muda wa wiki 2, wakati mwingine zinaweza kuendelea kwa wiki hadi 6. Wagonjwa wanashauriwa kufika kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupimwa na kupatiwa dawa za kupunguza madhara kulingana na ishara zitakazoonwa na Daktari.

Maambukizi haya husambazwa kwa njia zifuatazo;

  • Kugusa machozi au matongotongo kutoka kwenye macho ya mtu mwenye maambukizi.
  • Kugusana mikono na mtu mwenye maambukizi halafu ukajishika machoni. 

Macho Mekundu Yanaonekanaje na Kujisikiaje?

Wakati mwingine, jicho lako linaweza kuwa jekundu mahali ambapo palipaswa kuwa kweupe. Hii inaweza kutokea pindi vimishipa vya damu vilivyopo ndani ya macho yako vimevimba kuliosababishwa na kukereketa kwa jicho. Pia, inawezekana kabisa kuwa vimishipa vidogo vidogo vimepasuka.

Ikiwa jicho lako limekuwa jekundu kutokana na jeraha, basi inawezekana kuwa jicho limefungua zaidi (dilate) vimishipa vya damu katika jicho lako ili kuruhusu damu zaidi kufika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuharakisha uponyaji kwani damu ndiyo nyezo inayotumika kwenye uponyaji ndani ya mwili wa binadamu. ufungukaji mkubwa wa vimishipa hivi ndiyo inayosababisha macho kuwa mekundu.

Kulingana na hali inavyoendelea, macho yako mekundu yanaweza kujisikia:

  • Halina shida yoyote, kwa wengi wenye hali hii hawawezi kujua kama wana jicho jekundu mpaka wajiangalie au waambiwe na watu wengine.
  • Kuwasha au kuwa na kero, mara nyingi kwa wale walipata maambukizi (infection).

Jinsi ya kujisaidia

Kumbuka kuwa, kuna aina nyingi sana za macho mekundu, baadhi yake unaweza kujitibia wewe mwenyewe nyumbani na nyingine utajitaji msaada wa haraka wa daktari.

  • Pata mapumziko ya kutosha.
  • Weka kitambaa kizito juu ya macho yaliyofungwa.
  • Fanyia massage ngozi ya juu ya jicho (eyelid)
  • Kwa utaratibu kabisa safisha ngozi ya jicho (eyelid) kwa kutumia maji safi.
  • Unaweza kuweka matone ya dawa za kawaida (OTC).
  • Wakati mwingine, mtaalam wa huduma ya macho anaweza kupendekeza na kutoa dawa za viua vijasumu (antibiotics), matone maalum ya macho, au dawa za kunywa.

Ni nini hatari au madhara yanayowezekana ikiwa macho mekundu hayatibiwi?

Kwa mara nyingi, macho mekundu si hatari na inaweza hata isiwe na haja ya matibabu. Hata hivyo, kuna hali zinaweza kuwa na athari kubwa zaidi na zitakuladhimu upate matibabu ya kina.

  • Ikiwa umekaa na jicho jekundu kwa zaidi ya siku moja au mbili, au ikiwa tatizo hili limempata mtoto mdogo, basi unashauriwa uwasiliane na mtoa huduma za afya kwa uangalizi zaidi.
  • Pia, unatakiwa kuwasiliana na mtoa huduma pindi unaposikia maumivu au jicho linatoa matongotongo au uchafu wowote.
  • Endapo jicho lako kuwa jekundu ni matokeo ya athari kubwa kwenye jicho, endapo utakaa nalo bila ya matibabu linaweza kupelekea matatizo makubwa ikiwemo kupoteza uwezo wa kuona.

Jinsi ya kuepuka macho mekundu.

Si rahisi kuepuka kila macho mekundu, lakini unaweza kupunguza uwezekano wa kupata macho mekundu kwa kufuata ushauri ufuatao;

  • Usipendelee kusugua macho kwa kutumia mkono. Uchafu na vijidudu (germs) vilivyopo kwenye mikono yako vinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ya jicho kuwa jekundu au kukereketa (irritation).
  • Kama unatumia lenzi za ndani ya macho, hakikisha ni safi na usiweke kupitiliza muda ulioshauriwa.
  • Kwa wadada, tumia njia sahihi kuondoa urembo (make up) na hakikisha macho yako yanabaki masafi.
  • Hakikisha unapata muda wa kupumzika kila utumiapo kompyuta. Usitumie kwa muda mrefu bila kupata mapumziko.
  • Epuka vitu vinavyoweza kupelekea jicho kukereketa kama vumbi,moshi nk.
  • Hakikisha unajenga desturi ya kunawa mikono kwa maji safi na yanayotiririka kwa sabuni mara kwa mara kuzuia kupata maambukizi.
  • Onana na daktari pindi unapoona unapata macho mekundu mara kwa mara au umepata macho mekundu yasiyoisha.
  • Usichangie vipodozi na vitu vingine unavyotumia kama vile taulo za karatasi au nguo au dawa za macho.
  • Funika mdogo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya ili kuzuia kuambukiza wengine.

Dalili za hatari

Ingawa macho mekundu huisha yenyewe baada ya muda, ila kuna wakati, macho mekundu ni ishara ya ugonjwa mkubwa.Wasiliana na daktari pindi unapoona;

  • Jicho linauma.
  • Umeanza kuwa na uono hafifu.
  • Macho yanakuwa yanaogopa mwanga kupitiliza (extra sensitive to light).
  • Una dalili zaidi ya wiki na zimekuwa zikiendelea kuwa mbaya.
  • Jicho limekuwa likitoa matongotongo yanayoganda kwenye kope.
  • Umepata homa au maumivu yanayoambatana na kujisikia vibaya.

Hakikisha unaenda hospitari haraka iwezekanavyo pindi unapoona moja ya dalili hizi;

  • Jicho linauma kupitiliza.
  • Unaogopa mwanga kupitiliza.
  • Jicho limevimba.
  • Unaona ukungu. 

Neno kutoka TanzMED

Kimsingi, karibu kila mtu kwa nyakati tofauti amewahi kupata changamoto ya macho mekundu. Kwa wengi wetu, macho mekundu haijawahi kuwa ni tatizo kubwa. Maranyingi husababishwa na mkereketo wa jicho na huondoka pindi mkereketo unapoisha wenyewe. Lakini, kuna wakati kwa baadhi ya hali utatakiwa kwenda kuonana na daktari kwa vipimo zaidi. Hakikisha unawahi hospitali pindi unapoona maumivu ya jicho au changamoto kwenye uono (vision). Ni maamuzi ya busara kupata ushauri wa daktari pindi unapokuwa na changamoto ambayo hauna uhakika nayo. TanzMED inakuwezesha kuweka miadi na kuongea na daktari moja kwa moja kwa njia ya mtandao. Pakua TanzMED App na uweke miadi leo.

 

Baadhi ya vifungu vimekopiwa kutoka vipeperushi vya Elimu ya Afya kwa uma  https://elimuyaafya.moh.go.tz/