Image

Korodani Bandia Kutengeneza Shahawa?

Wanasayansi nchini Marekani wako mbioni kutengeneza korodani bandia (artificial testicle) zitakazokuwa zikitengeneza shahawa ili kusaidia wanaume wenye matatizo ya uzazi.

Timu ya wanasayansi katika jimbo la San Fransisco nchini Marekani chini ya Dk Paul Turek wamepewa ruhusa ya kuendelea na utafiti huu baada ya kuahidiwa kupewa pesa za kutosha kutekeleza mradi huu.

Kwa muda mrefu, wanasayansi wamejaribu kutengeneza seli za shahawa (Sperm Cells) bila mafanikio kwa vile wamefanikiwa kutengeneza robo tatu tu ya mchakato wa kupata shahawa kamili. Hii inatokana na mazingira maalum yanayopatikana katika korodani kuhitajika kukamilisha utengenezaji wa shahawa hizo. Mazingira hayo ya uhalisia ni tofauti na mazingira yoyote yale ya nje katika utengenezaji shahawa.

Korodani hizo zitakuwa katika umbo la duara (cylindrical shape) na zitakuwa na urefu wa inchi kadhaa na hazitahitaji kupachikwa kwenye mwili wa binadamu. Aidha kifaa hiki kitakuwa tofauti na korodani nyingine bandia ambazo huwekewa wanaume waliokosa korodani moja kutokana na sababu mbalimbali.Kwa kawaida korodani za namna hii huwa hazitengenezi shahawa kwa vile hujazwa maji maalum ya saline solution ili kutumika kama mapambo.

Ili kufanikisha hili, wanasayansi hao itabidi kubuni utaalamu wa kutengeneza chembechembe za shahawa na wamepanga kutumia seli za asili (human embryonic stem cells) zilizoongezewa jena (genes) ili kuzifanya kuwa seli zinazoweza kuzaa chembechembe za shahawa na hivyo kutumika katika njia za kutungisha mimba kwenye maabara zinazojulikana kama In Vitro Fertilization (IVF).

Wakati tafiti zimeonesha ya kwamba inawezekana kutibu panya dume mwenye matatizo ya uzazi kutoka katika seli zao za asili yaani embryonic stem cells, kwa binadamu tafiti hizi zimeshindwa kuzaa matunda yoyote yale mpaka sasa.

Kyle Orwig, Profesa wa masuala ya  uzazi na  magonjwa ya wanawake (Obstetrics and Gynecology) na sayansi ya uzazi (Reproductive Sciences) anasema “Ni mradi wa matumaini sana lakini nina wasiwasi kama utafanikiwa, ukifanikiwa itakuwa ni mafanikio makubwa sana katika sayansi ya tiba ya uzazi.” Kwa kawaida, shahawa hutengenezwa na kuhifadhiwa katika korodani za mwanaume.

Matatizo ya kushindwa kutungisha mimba kwa wanaume hutokana na hitilafu katika mfumo wa uzalishaji shahawa kwenye korodani unaosababishwa na magonjwa ya cystic fibrosis, matatizo ya jena (genetic defects), korodani ambazo hazijashuka katika sehemu sahihi (undescended testis), madhara katika korodani kama ajali na saratani ya kwenye korodani.

Kwa habari na matukio ya kila siku tembelea www.ughaibuni.com

 

 

 

 

 


Imesomwa mara 29409 Imehaririwa Jumatano, 12 Desemba 2018 11:13
Dr Khamis

Dr. Khamis H.Bakari (MD PhD) ni daktari bingwa,mhadhiri katika chuo cha afya cha Chuo  Kikuu cha Dodoma,mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya nyuklia (Nuclear medicine).

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.